Ulikuwa mchezo uliowaacha Wajerumani meno yote nje kwa bashasha na kuibua matumaini ya taifa zima kwamba timu yao ´Die Mannschaft´ inaweza kuwatoa kimasomaso katika michuano hiyo iliyoanza usiku wa kuamkia leo mjini Munich.
Goli la dakika za mwanzo mwanzo la Florian Wirtz na lile la katikati mwa kipindi cha kwanza liliofungwa na Jamal Musiala yalitoa ishara za mapema kabisa kwamba timu hiyo mwenyeji ingekuwa na mwanzo mzuri.
"Hakika hii ndiyo namna tuliyotaka kufungua michuano hii na kusema kweli tulihitaji mwanzo wa aina hiyo," amekaririwa nahodha wa kikosi cha Ujerumani Ilkay Gündogan alipozungumza na Kituo cha Utangazaji cha Taifa, ZDF.
Matarajio ya kabla ya michuano hii miongoni mwa Wajerumani yalikuwa madogo ikitiliwa maanani kwamba timu yao ya taifa ilivurunda vibaya sana katika mashindano matatu ya mwisho ya kandanda.
Lakini kwa mchezo waliouonesha usiku wa kuamkia leo vijana wa kocha Julian Nagelsmann wamefufua matumaini ya taifa zima kwamba huenda wanaweza kuja kucheza fainaliza Euro wiki nne zinazokuja mjini Berlin.

Post a Comment