Maafisa wa Upelelezi kutoka Kitengo cha Kupambana na Dawa za Kulevya (ANU) kilicho chini ya Makao Makuu ya Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), wamewakamata watuhumiwa wanne, wakiwemo raia wawili wa kigeni, kufuatia operesheni iliyofanikishwa kwa kutumia taarifa za kiintelijensia dhidi ya biashara ya dawa za kulevya jijini Nairobi.
Wakitekeleza taarifa za kuaminika walizopokea, maafisa hao walivamia nyumba iliyopo katika Jengo la Denluck Apartment majira ya saa 1:30 usiku (1930hrs), ambapo walifanikiwa kuwakamata Gabriel Moses Mathai (26), Gerald Otieno (28), Danilo Pejevic (25), raia wa Serbia, pamoja na Lukundo Samuel Sikombe (25), raia wa Tanzania.
Katika operesheni hiyo, wapelelezi walikamata kiasi cha dawa zinazoshukiwa kuwa bangi (Cannabis Sativa) katika mfumo wa majani makavu ya kijani yaliyokuwa yamefichwa ndani ya beseni la rangi ya buluu na mfuko mweusi wa plastiki.
Pia, ndani ya nyumba hiyo walipata vifaa mbalimbali vinavyoshukiwa kutumika katika usindikaji, ufungashaji na usambazaji wa dawa za kulevya. Vifaa hivyo ni pamoja na mizani ya kupimia, mkasi mmoja, viberiti vya kuwashia moto vitatu, karatasi za kufungia sigara aina ya Rizla, kifaa cha kusagia, vifaa vya kukunjia sigara na bahasha ndogo kadhaa zinazotumika kufungashia dawa hizo.
Watuhumiwa hao walipelekwa katika Kituo cha Polisi cha Muthaiga ambako wanashikiliwa kwa sasa wakisubiri kukamilika kwa uchunguzi na kufikishwa mahakamani.
Vielelezo vyote vilivyokamatwa vimehifadhiwa na kuhamishiwa Makao Makuu ya DCI kwa ajili ya uhifadhi salama, kurekodiwa na kufanyiwa uchunguzi wa kisayansi huku uchunguzi ukiendelea.
Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) imesisitiza kuwa itaendelea kwa dhati kupambana na biashara na matumizi mabaya ya dawa za kulevya na vilevile inawahimiza wananchi kutoa taarifa zitakazosaidia katika operesheni zinazoendelea dhidi ya uhalifu huo.







Post a Comment