Wananchi Wamlilia Lukuvi: “Alituwezesha Kupata Hati za Ardhi na Kututetea Wanyonge”



Na Usa River Media

Wananchi wa Jimbo la Isimani na maeneo jirani ya Mkoani Iringa wameelezea simanzi kubwa kufuatia kifo cha aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu) na Mbunge wa Jimbo la Isimani, Marehemu William Lukuvi.

Wananchi hao wanamkumbuka Lukuvi kama kiongozi shupavu aliyewaletea maendeleo katika sekta mbalimbali, huku wakimsifu hasa kwa juhudi zake za kutatua migogoro ya ardhi na kuwezesha wananchi kupata hati za miliki.


Mwili Wawasili Idodi, Wananchi Wafurika Kwa Maombolezo

Mwili wa marehemu Lukuvi uliwasili Kijijini kwake Kata ya Idodi, Wilaya ya Iringa Vijijini tarehe 30 Machi, 2026, ambapo ndipo utakapozikwa baada ya ibada ya mazishi. Katika eneo hilo, wananchi wamemiminika kwa wingi wakiwa na huzuni na kumbukumbu za kiongozi huyo aliyewahudumia kwa dhati.


Wananchi Waelezea Kazi Zake

Akizungumza na waandishi wa habari, Bw. Kombo Jumbe, mmoja wa waombolezaji, alisema kuwa marehemu Lukuvi alikuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma za ardhi kwa urahisi.

“Marehemu Lukuvi alianzisha utaratibu wa kliniki za ardhi wakati akiwa Waziri wa Ardhi. Hilo lilituwezesha sisi kupata huduma kwa haraka hasa katika migogoro ya ardhi. Yeye ndiye aliyezindua upatikanaji wa hati za ardhi na kufanya zoezi hilo kuwa endelevu,” alieleza Bw. Jumbe.

Kwa upande wake, Bw. Frank Mbindile, mkazi wa Kijiji cha Magozi Wilaya ya Iringa, alimsifu Lukuvi kwa tabia yake ya kusikiliza na kutetea wananchi.

“Marehemu alikuwa ni mtu anayependa kusikiliza shida za watu – iwe ni makundi au mwananchi mmoja mmoja. Ni aina ya kiongozi anayeamini katika kusimamia mambo ya msingi kwa ajili ya maslahi mapana ya wananchi. Akizungumza jambo, alikuwa na uwezo wa kulisimamia. Wana Isimani tumepoteza kiongozi mkubwa na lulu kwa taifa,” alisema Bw. Mbindile.


Mchango Wake Kwa Taifa

Marehemu William Lukuvi amehesabiwa kuwa kiongozi mwenye uratibu na mtetezi wa wanyonge katika nyadhifa mbalimbali alizoshika serikalini. Wananchi wanamkumbuka kwa usimamizi wake thabiti katika sekta ya ardhi, ambapo alileta mageuzi ya kutoa hati za ardhi kwa wananchi wa kawaida na kupunguza migogoro ya ardhi nchini.


Usa River Media – Kuleta Habari na Fursa Karibu Nawe.

Post a Comment

Previous Post Next Post

Mobile Logo Settings

Usa River Tv