Shughuli za Kamati za Kudumu za Bunge zimeanza kufanyika Jijini Dodoma tarehe 1 Agosti, 2024 na zinatarajiwa kuendelea hadi tarehe 25 Agosti, 2024 kabla ya kuanza kwa Mkutano wa Kumi na Sita wa Bunge ambao unatarajiwa kuanza kufanyika siku ya Jumanne tarehe 27 Agosti, 2024.
Shughuli zitakazotekelezwa wakati wa Vikao vya Kamati za Bunge katika kipindi hicho ni kama ifuatavyo:-
a. Kuchambua Miswada ya Sheria
Shughuli hii itatekelezwa na Kamati nne (4) za Bunge ambazo ni Kamati ya Utawala, Katiba na Sheria, Kamati ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Kamati ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo na Kamati ya Miundombinu.
b. Kuchambua Sheria Ndogo
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo, itafanya Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni katika Mkutano wa Kumi na Tano pamoja na kuchambua taarifa za Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge yatokanayo na Uchambuzi wa Sheria Ndogo zilizowasilishwa Bungeni katika Mkutano wa Kumi na Mbili na Kumi na Tatu.
c. Kupokea Taarifa za Utendaji wa Serikali na Taasisi zake
Kamati kumi na moja (11) za kisekta zitapokea na kujadili taarifa mbalimbali za utendaji wa Serikali na Taasisi zake.Aidha, Kamati ya Bajeti itapokea taarifa mbalimbali kutoka Serikalini kwa lengo la kufuatilia utekelezaji wa shughuli za Wizara ya Fedha na masuala yanayohusu vyanzo vya mapato ya Serikali.
d. Kuchambua Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali
Kamati mbili (2) zinazosimamia matumizi ya fedha za umma, zitachambua Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kuhusu Hesabu za Wizara, Mashirika ya Umma na Mamlaka za Serikali za Mitaa zilizokaguliwa kwa Mwaka wa Fedha ulioishia tarehe 30 Juni, 2023.
e. Kuchambua Taarifa za Uwekezaji wa Mitaji ya Umma
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) itapokea na kuchambua taarifa za uwekezaji wa mitaji ya umma ili kubaini iwapo uwekezaji huo una ufanisi na kwamba umezingatia taratibu na miongozo mujarabu ya biashara.

Post a Comment