Mhe. Majaliwa alitoa wito huo wakati akihutubia kwenye hafla ya Kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Anwani za Makazi, iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete (JKCC).
"Tunazo taarifa kwamba, vibao vya Anwani za Makazi tulivyoviweka kwenye mitaa na barabara, vimekuwa vikiondolewa na watu wasio waaminifu na kuuzwa. Watanzania, Serikali imetumia gharama kubwa katika kuanzisha mifumo hii. Ni jukumu letu sote kuhakikisha kuwa tunalinda miundombinu hii," alisisitiza Waziri Mkuu.
Aidha, Mhe. Majaliwa aliagiza Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuhakikisha kuwa maandalizi ya Sheria ya Anwani za Makazi yanaendelea kwa kasi, ili kurahisisha matumizi ya Anwani za Makazi kwa wananchi wakati wa kutoa na kupokea huduma mbalimbali, hasa zinazohitaji kutambulisha anwani.
Pia, alitaka Wizara hiyo kufanya maadhimisho ya Wiki ya Anwani za Makazi kuwa ya kimataifa kwa kuwashirikisha nchi jirani na za kimataifa.
"Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari inapaswa kushirikiana na wadau mbalimbali kutoa vishikwambi kwa watendaji wa kata, mitaa, vijiji na shehia, ili kurahisisha utendaji kazi katika ngazi hizo," aliongeza Waziri Mkuu.
Aidha, Mhe. Majaliwa aliagiza Ofisi ya Rais – TAMISEMI kusimamia utekelezaji wa mfumo wa Anwani za Makazi katika ngazi za Mikoa na Halmashauri, ikiwa ni pamoja na kuteua waratibu wa mfumo huo na kuwapa mafunzo ya kutosha.
Kwa upande wa Wizara ya Fedha, Waziri Mkuu alitaka ishirikiane na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuboresha Mfumo wa NaPA kwa kuongeza moduli mpya itakayohusiana na vyombo vya moto. Pia, aliagiza Wizara za Uchukuzi, Ujenzi, na Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kushirikiana kuhakikisha magari ya Serikali yanafungwa mfumo wa NaPA, na kuhimiza watoa huduma za usafirishaji kutoka sekta binafsi kufunga mfumo huo ili kurahisisha utambuzi wa maeneo mbalimbali nchini.
Kwa upande wake, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Jerry William Silaa (Mb), alisema kuwa Wizara yake, kwa kushirikiana na OR-TAMISEMI, imejipanga kuhakikisha mfumo wa Anwani za Makazi unakuwa endelevu.
"Tutaendelea kufanya uhakiki wa taarifa, kujenga uwezo kwa watendaji wa Serikali za Mitaa, kutunga Sheria ya Anwani za Makazi, kuboresha Mfumo wa kidijitali wa NaPA, na kuhamasisha matumizi ya Anwani za Makazi," alisema Mhe. Silaa.
Hafla hiyo iliongozwa na mada kuu ya "Anwani za Makazi: Msingi wa Maendeleo Endelevu," ikilenga kuhakikisha kuwa mfumo huo unatumika kikamilifu na kuleta manufaa kwa wananchi na taifa kwa ujumla.

Post a Comment